Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kimeweka mkakati wa kukagua magari ya shule yanayobeba wanafunzi.
Mkuu wa kikosi hicho, Marson Mwakyoma alisema licha ya magari yote kukaguliwa katika wiki ya nenda kwa usalama barabarani, utafanyika ukaguzi mwingine kuanzia leo kubaini magari yenye makosa.
“Kuna njia tatu za ukaguzi, kwanza ni ule wa kupeleka gari kituoni na kukaguliwa ambapo wamiliki wa shule wameshafanya. Nyingine ni ile ya kushtukiza ambayo tunakusimamisha ili kukukagua, ya mwisho ni ukaguzi maalumu ambao unahusisha magari yanayotoa huduma maalumu,” alisema Mwakyoma.
Alisema magari ya wanafunzi ni lazima yawe na vifaa vya kuwekea taka pamoja na waangalizi wa watoto, ambao pia wanapaswa kubeba jukumu la kuwavusha barabara.
“Ukaguzi huo pia, utahusisha uwezo wa dereva katika kuwaendesha watoto,” alisema.
Pia, alitoa wito kwa wazazi na walezi kupakia watoto maeneo salama ili kuepusha ajali.
Alipoulizwa kuhusu wanafunzi wasiopanda magari ya shule na wanasoma katika shule za mbali na kulazimika kuvuka barabara, alisema wameandaa dawati maalumu kwa ajili ya kutoa elimu kwa wanafunzi pamoja na kuwa na vipindi shuleni.
BOFYA HAPA KU DOWNLOAD APPS YA LINK CLASSIC USOME HABARI KIRAHISI NA HARAKA ZAIDI
CODE HAPA
No comments: