Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewanusuru viongozi 19 wa vyama vikuu vya ushirika vya mikoa ya Shinyanga (Shirecu) na Mwanza (NCU) kwenda rumande badala yake amewapa siku 23 wampe maelezo yatakayomridhisha kuhusu mahali zilipo mali za vyama hivyo viwili.
Majaliwa alifikia uamuzi huo jana wakati akifunga kikao cha wadau wa pamba alichokiitisha mkoani Shinyanga.
Viongozi hao wanatuhumiwa kwa upotevu wa mali zilizokuwa zikimilikiwa na vyama hivyo vya ushirika.
“Nataka kila mtu akaandae taarifa kuhusu mali za ushirika zilipo, au zimeenda wapi na kama mlizikopea, mseme ni wapi, lini na kwa ridhaa ya nani. Nataka maelezo ya kutosha kuniridhisha mali za ushirika zimeenda wapi,” alisema Waziri Mkuu katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake jana.
Alisema, “Hawa nitakaowataja walipaswa kuchukuliwa na RPC, wakatoe maelezo yao na hatua dhidi yao zichukuliwe. Sasa nataka nikutane nao Dodoma Januari 15, 2018 saa 3:30 asubuhi ofisini kwangu,” alisema.
Kuhusu tuhuma za viongozi wa NCU, Waziri Mkuu alisema chama hicho kati ya mwaka 2001 na 2017, kiliuza mali kinyemela katika mazingira yenye utata na kwa bei ndogo ikilinganishwa na thamani halisi.
Aliwataja viongozi waliohusika na upotevu huo ambao wanatakiwa kutoa maelezo kuwa ni Murtazar Alloo ambaye ni mnunuzi wa maghala matatu mali ya NCU; Samson Ng’halida (mnunuzi wa New Era Oil Mills); Amos Njite Lili (mnunuzi wa ghala la Igogo); Antonia Zacharia (mnunuzi wa jengo la Kauma); Timothy Kilumile (mnunuzi wa jengo la Kauma); Robert Kisena (mnunuzi wa pili wa New Era Oil Mills); Peter Ng’hingi (aliyekuwa mjumbe wa bodi); Daniel Lugwisha (aliyekuwa mhasibu mkuu - NCU); George Makungwi (aliyekuwa ofisa miliki - NCU) na Sospeter Ndoli (aliyekuwa ofisa utumishi -NCU).
Kuhusu mali za Nyanza zinazoshikiliwa na Benki ya CRDB, Waziri Mkuu alisema benki hiyo inaidai NCU mikopo yenye thamani ya Sh2.123 bilioni na kwamba inashikilia mali 16 zenye thamani ya Sh18.132 bilioni.
Alitaka vyombo vya dola vifanye uchunguzi ili kubaini uwiano wa mikopo na mali zinazoshikiliwa na benki.
Kwa upande wa viongozi wa Shirecu, alisema wanatuhumiwa kwa upotevu wa zaidi ya Sh11 bilioni ambazo wanadaiwa na Benki ya TIB yakiwamo madeni ya mishahara ya watumishi ambayo yanafikia Sh1.2 bilioni.
“Shirecu kwa sasa haina mali zozote kwa sababu zinashikiliwa na TIB kutokana na mikopo,” alisema.
Aliwataja viongozi wa Shirecu ambao wanatakiwa kutoa maelezo kuwa ni Joseph Mihangwa (meneja mkuu); Sillu Mbogo (kaimu mhasibu mkuu); Maduhu Nkamakazi (kaimu mkaguzi wa ndani); James Kusekwa (kaimu meneja uendeshaji).
Wengine ni wajumbe wa bodi ya Shirecu Robert Mayongela (mwenyekiti); Mary Mabuga (makamu mwenyekiti); Sigu Maganda (mjumbe); Clement Bujiku (mjumbe) na Charles Lujiga.
KWA HABARI ZAIDI
BOFYA HAPA KU DOWNLOAD APPS YA LINK CLASSIC USOME HABARI KIRAHISI NA HARAKA ZAIDI
CODE HAPA
No comments: