Biashara ya mtandao ni moja ya biashara zinazokua kwa kasi kubwa zaidi katika karne tuliyo nayo sasa. Imeonekana kuwa makampuni yanayofanya biashara hizi yana tabia ya kukua kwa kasi sana na kudumisha ukuaji huo kwa muda mrefu zaidi kuliko makampuni ya biashara za kawaida.
Hadi kufikia 2011, biashara za mtandao zilikaridiwa kufikia kuwa na thamani dola bilioni 100 zikiwa zinatengeneza faida kubwa sana. Haikushangaza kumsikia tajiri mkubwa duniani, Bill Gates, anayemiki kampuni ya software za kompyuta akisema kuwa kama ataruhusiwa kuanza upya biashara, atafanya biashara ya mtandao (network marketing). Katika mada hii tutazizungumzia faida za kufanya biashara hizi za mtandao.
Lakini kabla ya kuanza kuziorodhesha faida hizo tupate maneno machache kuhusu tabia ya biashara hii. Watu wengi huchukulia kwamba biashara hizi ni kimbilio baada ya kushindwa vitu vingine. Napenda kuwashauri kuwa hizi ni biashara kama nyingine zo zote, zinahitaji uwekezaji wa muda, nguvu na pengine pesa. Zina tabia tofauti kidogo na biashara zingine au kazi nyingine za ajira. Wakati hazihitaji mtu kuwa na cheti cha masomo, zinahitaji mwanachama
kuwa na tabia tofauti kidogo na ya mtu aliyezoea kuajiriwa. Hizi ni biashara ambazo mtu anayeshiriki atakuwa mwamuzi wa kila jambo linalohusu biashara yake, akishaanza kufanya biashara hii hakutakuwepo na mtu wa kumsukuma.
Kwa hiyo, zinahitaji mtu awe na uwezo wa kuwa na maamuzi sahihi na kufanya kazi kwa kujipangia mwenyewe. Watu waliofanikwa mapema na kwa kiwango cha juu ni wale waliokuwa na morali ya juu, waliofanya kazi bila kupumzika wakiwa wamejiwekea malengo yao. Hizi ni biashara ambazo unatakiwa kila wakati uzifikirie na kufanya jambo fulani kusogeza gurudumu lako mbele. Unatakiwa kujifunza sana kutoka kwa wale waliokutangulia na wengine wengi
waliokwisha fanikiwa katika biashara hizi.
Kwa vile ni biashara ambazo hazileti utajiri ghafla, zinahitaji uvumilivu wa hali ya juu mwanzoni na kusimama kwenye malengo uliyojiwekea bila kuyumba. Zina tabia ya kuanza kuonyesha matunda taratibu na kuongeza kasi kadiri unavyopanda ngazi kwenye kampuni yako. Ukifika juu, uzito wa kazi hupungua na unaanza kuishi kwa mtindo wa maisha waishio matajiri na watu walio maarufu.
Sasa tuone ni faida gani zinapatikana kutokana na kufanya biashara hizi za mtandao. Kuna faida nyingi sana za kufanya biashara ya mtandao, lakini katika ukurasa huu tumechagua na kuelezea faida 10 tu:
1. Malipo Kutokana Na Kazi Ya Wanachama Wengine ( Leveraged Income):
Hii ndio faida kubwa kuliko zote na ndiyo maana hapa nimeiweka kuwa ya kwanza. Hebu fuatilia kwa nini nasema hivyo…..
Katika siku moja idadi ya saa inaeleweka na huwezi kuibadili. Katika saa hizo za siku moja unatakiwa ufanye kazi ya kukupatia kipato, upate muda wa kulala, upate muda wa kuwa na familia na muda mwingine kwa ajili ya shughuli zako nyingine.
Fikiria muda wako wa kazi.
Watu wengi wanatakiwa kuwepo mahali walipoajiriwa kwa saa 8 kwa siku … kwenye kazi ambayo wanaifanya tu hata kama hawaipendi. Kwa kubadilishana na muda wao, waajiri huwalipa kiasi fulani cha pesa kwa kila saa aliyokuwepo kazini au kulingana na idadi fulani ya vitu alivyovizalisha. Hakuna malipo ya zaidi ya hapo. Kipato cha mwajiriwa huyu kimefungwa au kimewekewa ukomo kwa sababu;
Kwanza: Kuna ukomo wa idadi ya saa za kufanya kazi, na
Pili: Kuna ukomo wa idadi ya vitu unavyoweza kuvizalisha wewe peke yako katika muda uliopangiwa.
Kwa upande wa pili, tutazame biashara ya mtandao.
Biashara za mtandao huwalipa wanachama wao kutokana na kazi za wanachama wengine. Kwa hiyo basi, mwanachama ambaye ameweza kuongeza idadi ya wanachama walio chini yake atalipwa zaidi, na kila atakapowaongeza zaidi, atazidi kulipwa zaidi.
Uzuri uliopo hapa ni kuwa unaweza kuongeza idadi ya wanachama chini yako bila kuhitaji kuongeza muda wako wa kufanya kazi. Unaweza kupunguza muda wa kufanya kazi na bado ukaona kipato chako kikiongezeka. Ulipwaji kutokana na watu uliowasajili chini yako na kuwafundisha (leveraged income) ndio unaoifanya kuwa faida ya kwanza kwenye orodha hii.
2. Malipo Endelevu Kwa Kazi Ya Mara Moja (Passive Residual Income):
Kampuni za mtandao zinawapa fursa wanachama wao kupata malipo endelevu kwa kazi walizozifanya mara moja. Karibu kila mmoja wa watu wanaojiunga na biashara hizi huwa amevutiwa na aina hii ya malipo. Wewe kama mwanachama unamsajili mwanachama mara mmoja tu na mtu huyu akiendelea kununua bidhaa na kujenga timu inayofanya kazi vizuri, wewe utaendelea kulipwa tena na tena bila ushiriki wako wa moja kwa moja.
3. Mtaji Mdogo Wa Kuanzia:
Unaweza kuanza biashara ya mtandao kwa mtaji mdogo sana au kwenye kampuni nyingine bila kuwa na mtaji kabisa. Hakuna tofauti kati ya yule aliyenza na mtaji mdogo na yule aliyeanza na mtaji mkubwa, fursa zenu za kufika mnakotaka zinafanana na kubwa kuliko fursa utakayopata kwenye mifumo mingine ya biashara.
Pamoja na kuwa pengine utaanza biashara yako bila mtaji wo wote, utahitaji kiasi fulanai cha pesa kwa ajili ya uendeshaji wa biashara yako ikiwa ni pamoja na kununua bidhaa, mawasiliano, usafiri, matangazo n.k.
Nchini Tanzania, kuna dada ambaye alianza biashara kwa kutoa kiingilio cha Tshs 24,000/= kwenye kampuni ya Green World (kampuni inayohusu afya ya binadamu), akaanza kwa kupeleka wagonjwa kupata tiba kwenye kampuni hiyo na kukua taratibu hadi kufikia kupata bonasi nzuri kila mwezi na kupewa tuzo ya gari lenye thamani ya milioni 18 katika kipindi cha mwaka mmoja tu – hakuwa na mtaji zaidi ya pesa ya kiingilio.
4. Biashara Ya Kimataifa:
Kampuni nyingi za mtandao zinaruhusu wanachama wao kufanya biashara kimataifa. Hili linawezekana kwa kutumia mtandao. Unaweza kumsajili mwanachama kutoka nchi yo yote duniani na ukapata kipato kitakachotokana na kazi anayoifanya mwanachama huyu huko aliko. Kwa hiyo unaweza kujijengea biashara kubwa,
katika nchi tafauti, wewe ukiwa ndani ya nyumba yako.
5. Mafunzo
Biashara za mtandao hazihitaji uwe na uzoefu wa kuuza, wala hazihitaji uwe umepata mafunzo ya biashara. Kuwa na uzoefu huo au mafunzo hayo ni kitu kitakachokusaidia, lakini kila mwanachama anayejiunga na biashara hizi hupewa mafunzo ya kutosha. Mafunzo hayo utayapata kutoka kwenye kampuni au kutoka kwa mtu wa juu
yako (aliyekusajili). Kampuni nyingine hutoa mafunzo ya aina mbali mbali kwa wanachama wao, hutoa mafunzo darasani, CD, DVD, vipeperushi na hata vijitabu vya kujisomea.
6. Uhuru:
Kitu kibaya sana kwenye biashara za aina nyingine ni kukosa uhuru na hasa uhuru wa muda. Kazi nyingi zinakutaka ufanye kazi – saa 9 kwa siku, siku 5 kwa wiki – na unapata kipato kwa kuuuza muda huo kwa wiki. Huwezi kujiamulia ufike kazini saa ngapi. Mwajiri wako ndiye anayekupangia nini cha kufanya na wakati gani ukifanye.
Biashara ya mtandao unakuondolea vikwazo vyote hivi. Kuanzia siku ya kwanza unapoanza biashara ya mtandao, unajipangia ufanye kazi na nani… utakataka ufanye kazi muda gani… na utapenda kufanyia wapi kazi yako.
Una uchaguzi wa namna utakavyopenda kufanya biashara yako: kuongea na watu moja kwa moja; kutumia barua pepe; kutumia simu yako ya mkononi, kuitisha mikutano n.k. Ni biashara yako na utaifanya unavyopendezewa ifanyike.
7. Kujiendeleza Binafsi:
Moja ya faida kubwa ya biashara za mtandao ni kujiendeleza kibinafsi. Wafanya biashara za mtandao ni viongozi makini. Katika kufanya biashara hizi utajiongea ujuzi mwingi na uzoefu mkubwa katika kuzungumza mbele ya kadamnasi, kutoa ushauri, kufundisha watu na namna ya kuishi na watu.
Kufanya biashara ya mtandao kunakuwezesha kufahamiana na watu wa mikondo mbalimbali ya kimaisha, kujipatia marafiki wapya na kujua mikondo mingine ya kibiashara.
8. Hakuna Ukomo Wa Kipato:
Hakuna kiwango cha mapato unachopangiwa kupata. Katika kazi au biashara nyingine za kawaida kiwango chako cha mshahara kimepangwa na hakiwezi kuwa zaidi kwa elimu na ujuzi ulio nao.
Hivyo sivyo katika biashara za mtandao. Wewe ndiye utakayejipangia kiwango unachopenda kukipata, kampuni haina
pingamizi la namna yo yote kama ilivyo kwenye makampuni ya kawaida.
Ukishapata ujuzi wa kufanya biashara ya mtandao, utapata kipato cho chote kulingana na uvumilivu wako na kujituma kwako katika kuwasaidia wengine.
9. Unafanya Biashara Po Pote:
Maendeleo ya teknolojia yanamwezesha mfanya biashara ya mtandao kufanya shughuli zake po pote alipo. Ukiwa na simu ya kiganjani unaweza kuwasiliana na wateja wako kutoka po pote ulipo.
Ukiwa umeunganishwa kwenye internet, unaweza kuchukua simu yako au lap top yako na ukaendelea kufanya biashara zako ukiwa safarini, ukiwa kwenye mapumziko, ukiwa umekwenda kuwaona ndugu walio kwenye mji mwingine na hata ukiwa nchi nyingine.
10. Bidhaa Za Kipekee Na Zinazohitajika:
Baadhi ya bidhaa na huduma bora kabisa ulimwenguni hupatikana kwenye makapuni yanayofanya biashara ya mtandao. Bidhaa hizi haziuzwi kwenye maduka ya kawaida, na hata kama zingeuzwa
humo, hakuna mtu ambaye angezitambua. Bidhaa ikiwa ni nzuri na ya kipekee, inahitaji mtu wa kuielezea, jambo ambalo haliwezekani dukani kutokana na uwingi wa bidhaa katika duka hilo.
Ni yule mtu aliyetumia bidhaa au huduma akaipenda, anayeweza kuuelezea uzuri wa bidhaa au huduma hiyo.
Katika mada yetu ya leo tumeona faida 10 zinazopatikana kwa kufanya biashara za mtandao.
Katika mada nyingine tumezungumzia maana ya biashara ya mtandao na namna biashara hizo zinazofanya kazi ili kuwafahamisha wale wasio na ufahamau na biashara hizi na kusahihisha mawazo potofu walio nayo wengi kuwa biashara hizi si za kweli au kuwa ni biashara kwa ajili ya watu walioshindwa vitu vingine vya kufanya katika maisha yao.
Tumeandika pia mada kuhusu namna ya kuchagua au vigezo vya kuvitumia wakati wa kuchagua biashara ya mtandao ya kujiunga nayo. Vile vile tuliandika kuhusu vitu vya kuzingatia ili uweze kunufaika zaidi na biashara ya mtandao ambayo umeshajiunga nayo.
KWA HABARI ZAIDI
BOFYA HAPA KU DOWNLOAD APPS YA LINK CLASSIC USOME HABARI KIRAHISI NA HARAKA ZAIDI
CODE HAPA
No comments: