Kutokana na kasi ya kuongezeka kwa idadi ya watu nchini, kasi ya ujenzi wa nyumba za kuishi imekuwa ikiongezeka siku hadi siku. Miji mingi nchini inakua kwa kasi kubwa. Kila mtu anataka kujenga nyumba au anajenga au ameshajenga nyumba yake inaweza ikawa mjini au kijijini.
Kutokana na kuongezeka kwa kasi hiyo Serikali iliamua kuandaa sheria zitakazoongoza umiliki wa viwanja na ujenzi wa nyumba. Kuna sheria ya Ardhi namba 4 na namba 5 ya mwaka 1999 inayotoa maelekezo ya namna ya umiliki wa ardhi pia kuna Sheria ya mipango miji namba 8 ya mwaka 2007 inayotoa maelekezo ya namna ujenzi wa nyumba na huduma za jamii utakavyokuwa katika maeneo ya mijini.
Kwahiyo unapotaka kujenga nyumba yako ili usije ukaathiriwa na sheria hizi wakati wa utekelezaji wake kuna mambo kadhaa unatakiwa kuyazingatia maana usipoyazingatia kuna hatari ya kupata hasara na tayari mpaka hivi sasa kuna watu wengi wamekumbwa na kadhia hii katika maeneo mbalimbali nchini.
1. Nunua Kiwanja Kilichopimwa au Hakijapimwa
Unapotaka kujenga nyumba katika eneo la mjini au eneo lililotangazwa kuwa eneo la mipango miji jambo la kwanza unatakiwa kununua kiwanja kilichopimwa. Kununua kiwanja kilichopimwa kunaondoa uwezekano wa kuja kubomolewa nyumba yako kwa sababu mji utakuwa umeshapangwa tayari. Lakini pia unapokuwa na hati yako ya kumiliki kiwanja inahalalisha kisheria umiliki wako wa kiwanja itakulinda popote kwenye swala linalohusu umiliki wa kiwanja chako.
Wakati mwingine kuna baadhi ya maeneo ya mjini hayajapimwa je, usinunue kiwanja? Au usijenge?. Jibu ni hapana, unaweza kununua na kujenga lakini kinachotakiwa kwanza uwasiliane na Ofisi ya Ardhi ya Halmashauri husika ukaulizie ikiwa mahali unapotaka kununua kiwanja hicho hawajapanga matumizi mengine tofauti na makazi. Nasema hivyo kwa sababu unaweza kununua kiwanja kwenye eneo ambalo wanalifikilia au wamelipangia matumizi mengine mfano viwanda, au dampo la takataka halafu mara unapomaliza kujenga unaambiwa hili ni eneo la viwanda na unatakiwa kuhama, waswahili wanasema itakula kwako.
Ukisha jiridhisha kutoka kwa wataalamu wa ardhi, sasa unaweza kununua kiwanja hicho. Usifanye haraka kununua kiwanja kisa unauziwa kwa bei nafuu jiridhishe kwanza ndipo ununue. Wakati unanunua ni muhimu sana kuzingatia jambo la pili linalofuata.
2. Wasiliana Na Uongozi Wa Mtaa Hasa Mwenyekiti Wa Mtaa Na Balozi
Watu wengi sana wanafanya makosa ya kutowashirikisha viongozi wa mtaa wakati wa kununua kiwanja. Unakuta mtu anakuja na mahela yake amepata kwenye dili huko haraka haraka anaongea na mwenye kiwanja analipa pesa kisha anapotelea zake huko. Kununua kiwanja bila kuwashirikisha viongozi wa mtaa unaweza kuuziwa kiwanja kilichouzwa kwa mtu mwingine mkajikuta mnamiliki kiwanja kimoja watu watatu au wawili, hali hii imetokea sehemu nyingi sana ninauzoefu na hilo.
Viongozi wa mtaa ni muhimu sana kuwashirikisha maana wao mara nyingi huwa wanaaalikwa kwenye mauziano ya viwanja vya watu wao wa mtaa, kwahiyo viwanja vingi wanawafahamu wamiliki wao. Ukitaka ujiridhishe zaidi ni vizuri kama utawapata majirani wa kiwanja unachotaka kununua itakuwa jambo jema maana watakuhakikishia mipaka ya kiwanja unachonunua. Kumbuka kuandikiana mkataba wa mauziano na mashahidi wawepo na wasaini kwenye mkataba huo ili mambo yakigeuka baadae usiumie.
Ukiwa na viongozi wa mtaa, hakikisha kiwanja chako kina barabara inayofika kwenye kiwanja hicho au hakikisha hakiko karibu sana na barabara kiasi kwamba baadae kinaweza kukatwa ili kupisha barabara. Kitu kingine cha muhimu kwenye maeneo ambayo hayajapimwa waulize viongozi wa mtaa wamependekeza barabara ipitie sehemu gani na itakuwa na upana gani, hapa kwenye upana kama ni barabara ya mtaa hakikisha isipungue mita kumi ili ramani ya mipango miji itakapo chorwa isikuathiri sana.
3. Mara Tu Unapomaliza Kununua Kiendeleze Kiwanja Chako
Kiendeleze kiwanja kwa kupanda miti, kuweka fensi au nguzo kwenye kila kona ya kiwanja ili watu wengine wasije wakakuingilia. Hakikisha unafanya mapema sana kukiendeleza kwa sababu ukichelewa kidogo tu unaweza kukuta migogoro mia kasoro. Nakushauri upande miti mingi uwezavyo kwenye kiwanja kwa kufuata “landscape” unayoweza kuiandaa wewe mwenyewe au ukawapa wataalamu wakakuandalia.
Faida ya kupanda miti mapema ni kwamba ikitokea kuna mabadiliko kwenye ile ramani ya mipango miji lile eneo likapangiwa matumizi mengine watabidi wakulipe fidia. Fidia huwa kubwa ikiwa kwenye kiwanja kuna miti mingi maana kila mti hulipwa fidia. Faida nyingine ya kupanda miti ni kutengeneza mandhari nzuri ya kuishi punde utakapo maliza ujenzi na kuhamia pale.
Tahadhari; Usikiache kiwanja kiko tupu kwa muda mrefu maana utashangaa kila mtu anajiongezea eneo kwenye kiwanja chako.
4. Andaa Ramani Ya Nyumba Utakayoijenga.
Unatakiwa kuwa na ramani ya nyumba utakayo ijenga. Ramani unaweza kuipata kwa mtu yeyote anayechora ramani za nyumba mfano anaweza kuwa Msanifu ramani, au msanifu majengo, anaweza kukuchorea ramani nzuri.
Kama unajenga nyumba kwenye kiwanja kilichopimwa, unatakiwa kupata kibali cha ujenzi wa nyumba kutoka ofisi za ujenzi za halmashauri husika.
5. Anza Kujenga Nyumba Yako Lakini Zingatia Vipimo Hivi.
Hakikisha nyumba unayoijenga kama kiwanja chako kiko pembeni ya barabara isiwe karibu na barabara yaani nyumba yako isogeze nyuma ya kiwanja. Unataikiwa kufanya hivyo ili wakati mwingine kuna mabadiliko ya upanuzi wa barabara kwahiyo kama nyumba yako iko karibu ya barabara inaweza ikalazimika kubomolewa lakini kama iko mbali na barabara inaweza kunusurika.
Pia unatakiwa uache mita moja na nusu kutoka kila upande wa mipaka ya kiwanja chako ili kuacha uchochoro kati yako na jirani yako.
Unashauriwa kuacha angalau mita tano au zaidi ya hizo kutoka barabarani kutegemeana na ukubwa wa kiwanja chako.
“Kwahiyo unapotaka kujenga nyumba yako ili usije ukaathiriwa na sheria hizi wakati wa utekelezaji wake kuna mambo kadhaa unatakiwa kuyazingatia maana usipoyazingatia kuna hatari ya kupata hasara na tayari mpaka hivi sasa kuna watu wengi wamekumbwa na kadhia hii katika maeneo mbalimbali nchini”
Tunakutakia kila la heri katika ujenzi wa Taifa.
Tunakuhamasisha ili ufikie mafanikio yako.
KWA HABARI ZAIDI
BOFYA HAPA KU DOWNLOAD APPS YA LINK CLASSIC USOME HABARI KIRAHISI NA HARAKA ZAIDI
CODE HAPA
No comments: