NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana amecheza kwa dakika zote 90 na kuisaidia klabu yake, KRC Genk kutinga fainali ya Kombe la Ubelgiji kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Kortrijk katika mchezo wa marudiano wa Nusu Fainali Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
Kwa matokeo hayo, Genk inasonga mbele kwa faida ya mabao ya ugenini baada ya sare ya 3-3 kufuatia awali kufungwa 3-2 kwenye mchezo kwanza Uwanja wa Guldensporen mjini Kortrijk.
Mfungaji wa bao pekee la Genk usiku wa jana ni kiungo Msenegali mwenye umri wa miaka 28, Ibrahima Seck aliyefunga dakika ya 15 akimalizia pasi ya kiungo Mspaniola, Alejandro Pozuelo Melero.
Genk sasa itakutana na mshindi wa jumla kati ya Club Brugge na Standard Liege zinazomenyana kesho Saa 4:45 usiku Uwanja wa Jan Breydelstadion mjini Brugge. Mechi ya kwanza Standard Liege ilishinda 4 – 1 na leo itakwenda kupigania sare au kufungwa si zaidi ya 2-0.
Samatta jana alikuwa anacheza kwa mara ya nne tangu apone maumivu ya mishipa midogo ya goti lake la mguu wa kulia iliyochanika Novemba 4, mwaka jana akiichezea KRC Genk ikilazimishwa sare ya 0-0 na Lokeren katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk na kumsababisha afanyiwe upasuaji mdogo.
Kwa ujumla Samatta amefikisha mechi 74 tangu alipojiunga na Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Na katika mechi hizo, Samatta, mshambuliaji wa zamani wa Mbagala Market, African Lyon na Simba za Tanzania, amefunga mabao 22 kwenye mashindano yote.
Kikosi cha KRC Genk kilikuwa; Vukovic, Uronen, Colley, Aidoo, Nastic, Wouters, Seck, Pozuelo/Writers dk79, Samatta, Buffel na Ingvartsen/Karelis dk65.
KV Kortrijk; Kaminski, Kumordzi, Makarenko, Kagelmacher, Rougeaux, Ajagun/Lepoint dk73, Chevalier, Van Der Bruggen/Azouni dk73, Ouali/Stojanovic dk84, D'Haene na Perbet.
BOFYA HAPA KU DOWNLOAD APPS YA LINK CLASSIC USOME HABARI KIRAHISI NA HARAKA ZAIDI
CODE HAPA
No comments: