Wakati wafanyakazi wa Wakala wa Barabara (Tanraods) wakiendelea kuweka alama kwenye nyumba zinazotakiwa kubomolewa kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro, wakazi wanaoishi kati ya Ubungo na Kimara wamelalamikia kitendo hicho.
Baada ya kutekeleza ubomoaji wa nyumba kati ya Kimara na Kiluvya zilizo ndani ya mita 121.5 kutoka katikati ya barabara hiyo, ubomoaji mwingine utazikumba takriban nyumba 1,200 zilizo ndani ya mita 90, zikiwemo tano za ibada, vituo vya mafuta na majengo ya biashara nyingine kama za starehe.
Ubomoaji huo pia utalikumba moja ya majengo maarufu ya makao makuu ya Shirika la Umeme (Tanesco) lililopo Ubungo.
Eneo hilo na mengine ndiyo yaliyozua utata mwaka 2011 baada ya kutangazwa ilani ya kubomoa nyumba zote zilizo ndani ya hifadhi ya barabara bila ya kulipa fidia na kumsukuma aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutangaza kusimamisha ubomoaji ili kusubiri uamuzi wa Baraza la Mawaziri.
Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete pia alisema bila ya kutaja eneo kuwa ubomoaji ni lazima uzingatie historia ya eneo husika na haki za binadamu kwa kutoa muda wa kutosha kwa wakazi ikiwa nyumba zao ni lazima zibomolewe kutokana na mipango ya Serikali.
Mpango huo ulisimama na sasa, miaka saba baadaye, ubomoaji huo umefufuliwa na wafanyakazi wa Tanroads wanapita maeneo hayo kuweka alama ya “X”.
Wakizungmza kwa nyakati tofauti, wananchi wa maeneo hayo waliiambia Mwananchi kuwa kitendo cha kubomoa nyumba zao kitawasababishia machungu kwa kuwa hawajui pa kwenda.
“Kubomoa nyumba kutanizidishia msongo wa mawazo. Mume wangu alifariki mwaka juzi na nimebaki na watoto watatu. Nategemea nyumba hii kama njia ya kuniingizia kipato,” alisema mkazi wa Kimara Baruti aliyejitambulisha kwa jina la Furaha Nassoro ambaye ameishi eneo hilo kwa miaka 12.
“Nimeweka wapangaji vyumba sita. Hii ndiyo ajira yangu, sina kazi wala biashara ngingine.”
Alisema wakati Tanroads wanakwenda kuweka alama, walimtaka awe ameondoka ndani ya mwezi mmoja, hali iliyompa wakati mgumu kwa kuwa hautoshi.
“Watoto wangu wote wanasoma kwa uhamisho wa harakaharaka hivi nawezaje kumudu gharama hizi? Mwezi ujao kama watakuja kubomoa, itabidi wanangu wasiende shule hadi hapo nitakapopata pesa kwa ajili ya kuhama,” alisema.
Alisema kinachofanyika ni kwa ajili ya maendeleo, lakini alidai kuwa maendeleo hayawezi kuja wakati wananchi wana machungu ya kubomolewa nyumba na badala yake kulala nje. Mkazi mwingine wa Ubungo, James Haule alisema alipokea kwa huzuni taarifa ya nyumba yake kuwekwa alama ya kutakiwa kubomolewa kwa kuwa alimaliza ujenzi wa nyumba hiyo mwishoni mwa mwaka jana.
Haule aliiomba Serikali kuongeza miezi mingine miwili.
“Mwezi mmoja dada hautoshi. Tuna watoto, tunasomesha, maisha yenyewe ya sasa kama unavyoyaona. Mwezi huu mmoja napata wapi pesa ya kupanga au Serikali inataka tuaibike?”alihoji.
Katika eneo jingine, Mwananchi ilimkuta mzee aliyejitambulisha kwa jina la Onesmo Mwinuka akiwa nje ya nyumba yake huku akitazama alama ya “X”, usoni akionekana kupoteza matumaini.
“Hivi si walishabomoa Kimara? Huku tena wanataka nini? Kwani eneo lote la Kimara halitakiwi kuishi mtu? Sisi ni wanyonge, Rais atuonee huruma,” alisema Mwinuka.
Alisema kwa kuwa lengo la Serikali ni kuleta maendeleo ya nchi, lakini pia iangalie namna ya kuwasaidia wazee kwa vile maisha yao yatakuwa hatarini watakapobomolewa.
Diwani wa kata ya Kimara, Pascal Manota alisema alishaongea na wananchi kuwataka wajiandae kulipokea suala hilo kwa kuwa haliwezi kuepukika.
Alisema kwa sasa anawashauri wananchi hasa wapangaji kulipa kodi ya muda mfupi ili kuepuka hasara baadaye kwa kuwa muda wowote huenda Tanroads wataanza kubomoa nyumba hizo.
“Wametoa notisi ya mwezi mmoja, kwa hiyo huenda mwezi ujao zoezi la kubomoa likaanza kwa hiyo nini cha kufanya ni kuwashauri tu wananchi wajipange na kuzoea hii hali,” alisema. Akizungumza na Mwananchi, meya wa Ubungo, Boniface Jacob alisema amewaambia wananchi wapeleke suala hilo mahakamani ili wapewe haki zao na atawatafutia mwanasheria.
Alisema kitendo cha kutoa mwezi mmoja ni kuwanyima haki kwa kuwa ilibidi wananchi wafuatilie kwanza kujua hatima yao.
Meneja wa Tanroads wa mkoa, Julius Ndymukama alisema uwekaji alama utafuatiwa na ubomoaji.
“Tumetoa notisi ya mwezi mmoja na baada ya hapo tutaanza kubomoa,” alisema.
KWA HABARI ZAIDI
BOFYA HAPA KU DOWNLOAD APPS YA LINK CLASSIC USOME HABARI KIRAHISI NA HARAKA ZAIDI
CODE HAPA
No comments: